Matukio

Habari

news image

DART kulipa fidia kwa kutekeleza mradi awamu ya pili

Wakati Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ukiwa karibu kuanza kazi ya usimamizi wa utekelezaji wa mradi wa awamu ya pili, hatua za kulipa fidia watu walioathiriwa na mradi maeneo ya Mbagala zinaanza.

Kazi ya kuanza kulipa fidia imebainishwa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Usafirishaji na Maendeleo wa Wakala wa DART Bw. Victor Ndonne wakati akizungumza na watu walioanishwa kulipa fidia ili kupisha mradi wa DART awamu ya pili katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa kazi ya kuhakiki na kuthamini fidia kwa wahanga wa mradi imekamilika.

Maeneo ambayo watu watalipwa fidia ni pamoja na Mbagala Rangi tatu, Mtoni Kijichi. Chuo cha Ualimu (DUCE) na Keko.

Kazi ya uhakiki na uthamini wa mali zitakazoathiriwa na mradi wa DART imefanya na Wakala wa DART kwa kushirikiana na maafisa kutoka Manispaa ya Temeke na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke.

Ulipaji wa fidia ambao unajumuisha wahanga 102, utafanywa kwa awamu nne ikianzia na watu 71 kutoka mtaa wa Mianzini na awamu ya pili watu sita (6) kutoka Kata ya Kijichi, Bwana Ndonne alisema.

Bwana Ndonne ameendelea kufafanua kuwa awamu nyingine ni eneo la viwanda ambalo liko mtaa wa Mianzini lenye watu 15 wa kulipwa fidia, na awamu ya nne inayohusisha barabara ya Kilwa, Chang’ombe, Chuo cha Ualimu (DUCE),bustani iliyoko kwa Azizi Ally na Temeke yenye watu 10 wa kulipwa fidia.

Mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa wale watu watakaolipwa fidia wanatakiwa kujiandaa kupisha maeneo hayo ili ujenzi wa miundombinu wa DART uanze.

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka unasimamia utekelezaji wa mradi wa DART ambao umepangwa kufanyika kwa awamu sita katika jiji la Dar es Salaam.

Ramani

    Hakuna Taarifa kwa sasa