Wakala wa DART na IFC waanzisha ushauri wa kitaalam kwa awamu mbili za BRT

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka -DART, kwa ushirikiano na Shirika la Kimataifa lenye kutoa Ushauri wa Kifedha-IFC, umezindua rasmi mchakato wa ushauri unaolenga kuwezesha ununuzi wa watoa huduma kwa Awamu za 3 na 4 za mfumo wa Usafiri wa Haraka wa Mabasi-BRT katika jiji la Dar es Salaam.
Mkutano wa uzinduzi, uliofanyika katika ofisi za DART zilizopo Dar es Salaam, uliwakutanisha wataalamu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na washauri wa kisheria, kiufundi, mazingira, na kijamii. Kikao hiki kilikuwa hatua muhimu katika juhudi za serikali za kuboresha usafiri wa mijini na kuvutia ushiriki wa sekta binafsi katika uendeshaji wa mfumo wa BRT.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka-DART, Dk. Athumani Kihamia, aliwakaribisha wajumbe wa IFC na kueleza dhamira ya IFC ya kushirikiana kikamilifu katika mchakato wa ushauri. “Tuko tayari kushirikiana na IFC na wadau wote muhimu ili kuhakikisha muundo mzuri wa biashara ya Ushirikiano wa Umma na Sekta Binafsi (PPP) kwa awamu zijazo za mradi wa DART,” alisema Dk. Kihamia.
Timu ya IFC iliongozwa na Jacques Bleindou, Afisa Mkuu wa Uwekezaji na Kiongozi wa Timu kutoka Kenya. Bleindou alieleza malengo makuu ya ushauri wa kitaalam, akisisitiza umuhimu wa kushirikisha wadau wengi ili kupata taarifa kamili kuhusu mradi wa BRT. “Ushauri huu kitaalamu utatupa uwezo wa kuunda mfano wa manunuzi ya watoa huduma ulio na ufanisi, endelevu, na wa gharama nafuu kwa watumiaji wa usafiri wa umma katika jiji la Dar es Salaam,” alisema.
Timu ya wataalamu wanaoshiriki katika ushauri inajumuisha Mshauri wa Kisheria kutoka Gide Loyretle Novel, ALN Tanzania; timu ya wataalam wa Kiufundi ikijumuisha Ingerop Conseil et Ingenierie, Espelia, ITDP, na Bene Consult Limited; na timu ya Wataalamu wa Mazingira na Jamii kutoka ESG Africa Limited na wataalamu wa ndani.
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Usafiri wa Wakala wa DART, Mha. Mohamed Kuganda, aliteuliwa kuwa mratibu wa mchakato wa ushauri wa kitaalamu. Kuganda alisisitiza jukumu la shirika hilo katika kuwezesha ufikiaji wa wadau muhimu na nyaraka za mradi. “DART imejizatiti kutoa msaada wote unaohitajika ili kuhakikisha mchakato unaoendeshwa kwa urahisi na kumwezesha IFC kutoa mapendekezo yenye taarifa sahihi,” aliongeza.
Mchakato wa ushauri utajumuisha mahojiano na taasisi mbalimbali za serikali na wadau, ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Rais – Tawala wa Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Wizara ya Fedha, Wizara ya Uchukuzi, Wakala wa Barabara Tanzani (TANROADS), na Kituo cha Ubia wa Uwekezaji (PPP). Ushirikiano huu ni muhimu ili kuoanisha mradi na sera za usafiri wa kitaifa na mifumo ya kifedha.
Wakala wa DART Pamoja na IFC wanatekeleza mradi wa BRT kwa kufuata mfano wa PPP wa kuvutia waendeshaji mabasi binafsi ambao watakuwa na jukumu la kufadhili, kuendesha, na kudumisha idadi ya mabasi ya BRT kwa Awamu za 3 na 4. Katika makubaliano haya, waendeshaji binafsi watanunua na kuendesha idadi tofauti za mabasi na mifumo ya uendeshaji, wakati serikali itakuwa na jukumu la kujenga miundombinu ya barabara na majengo yanayohusiana na BRT, kwa ufadhili wa mkopo wa Benki ya Dunia.
Awamu ya 3 ya mradi wa DART inaanzia katikati ya jiji hadi Gongolamboto kupitia Barabara ya Nyerere iendayo uwanja wa ndege; wakati Awamu ya 4 inaanzia katikati ya jiji hadi Bunju kupitia Barabara ya Bagamoyo. Awamu hizi ni sehemu ya mtandao wa BRT katika jiji la Dar es Salaam, ikiboresha usafiri wa jiji kwa maelfu ya wasafiri wa kila siku katika Dar es Salaam.
Kulingana na wataalamu washauri wa kiufundi wa IFC, kuanzishwa kwa watoa huduma wa sekta binafsi kunatarajiwa kuboresha ufanisi wa huduma, kuboresha idadi ya mabasi, na kuhakikisha uendeshaji wa kifedha endelevu wa mfumo wa BRT. “Tunalenga kuunda mfumo wa ununuzi unaohimiza uwekezaji wa katika sekta binafsi huku tukihakikisha gharama nafuu kwa wasafiri,” alisema mshauri wa kiufundi wa IFC.
Masuala ya mazingira na kijamii pia yalijadiliwa katika mkutano huo, ambapo ESG Africa Limited ilieleza athari zinazoweza kutokea na hatua za kupunguza athari hizo. “Kuhakikisha uendelevu wa mazingira na kijamii ni sehemu muhimu ya ushauri huu wa kitaalamu, na tutafanya kazi kwa karibu na wadau wote ili kuondoa hofu yoyote ile,” alisema mwakilishi kutoka ESG Africa Limited.
Awamu ya kwanza ya ushauri wa kitaalam inajumuisha ukusanyaji wa maoni kutoka idara za ndani ya Wakala wa DART na taasisi za serikali za serikali. Baada ya mkutano wa uzinduzi, timu ya IFC ilifanya mahojiano na idara na vitengo mbalimbali za Wakala wa DART ili kupata taarifa za awali kuhusu hali ya sasa ya mfumo wa BRT na mipango yake ya upanuzi wa baadaye.
Katika siku ya Januari 29, 2025, timu ya IFC ilielekea Dodoma, Mako Makuu ya Serikali ya Tanzania, kukutana na wadau muhimu kutoka wizara mbalimbali. Ushirikiano huu unatarajiwa kutoa mchango muhimu kwa mchakato wa muundo wa kutayarisha manunuzi ya watoa huduma kuhakikisha kuwa mifumo ya sera na mahitaji ya kisheria yanazingatiwa ipasavyo.
Kadri mchakato wa ushauri wa kitaalamu unavyoendelea, vikao vya ushirikiano vitafanyika, ikiwa ni pamoja na mashauriano na wadau kutoka sekta binafsi wanaoweza kuhitaji huduma kutoka taasisi za kifedha. Wakala wa DART utaendelea kuwa na jukumu kuu katika kuwezesha majadiliano na kuhakikisha kuwa mitazamo yote muhimu inajumuishwa katika mapendekezo ya mwisho.
Mradi wa BRT ni sehemu muhimu ya mkakati wa maendeleo ya miji ya Tanzania, ukilenga kutoa mfumo wa usafiri wa umma wenye ufanisi, wa kuaminika, na endelevu kwa idadi inayoongezeka ya watu katika jiji la Dar es Salaam. Kwa kutumia utaalamu na uwekezaji wa sekta binafsi, serikali inatarajia kuboresha ubora wa huduma huku ikipunguza gharama za uendeshaji.
Wakala wa DART una matumaini makubwa kuhusu matokeo ya ushauri wa kitaalamu wa IFC kwa awamu zijazo za mfumo wa BRT. “Hii ni hatua kubwa kuelekea kufikia maono yetu ya mfumo wa usafiri wa umma wa kiwango cha juu katika jiji la Dar es Salaam,” alisisitiza Dk. Kihamia.