Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
DART kusitisha matumizi ya tiketi za karatasi kuanzia mwezi Machi
07 Feb, 2025
DART kusitisha matumizi ya tiketi za karatasi kuanzia mwezi Machi

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART umesema kuanzia mwezi Machi mwaka huu wa 2025 utasitisha rasmi matumizi ya tiketi za karatasi katika usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka na badala yake watumiaji wote wa Mabasi watatakiwa kutumia kadi janja ambazo zinaendelea kuuzwa katika vituo vikuu vya mradi huo.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam wakati wa kuhitimisha mradi wa Maendelezo Yatokanayo na uboreshaji wa usafiri wa umma (TOD), Mtendaji Mkuu wa DART Dkt. Athumani Kihamia amesema ifikapo tarehe mosi mwezi Machi matumizi ya tiketi za karatasi katika kulipia nauli za mwendokasi yatasitishwa.

“Ni kweli tumeendelea kusisitiza watumiaji wa Mabasi yetu ya Mwedokasi wajitahidi kuwa na kadi janja na kuzitumia lakini hata hivyo baadhi yao bado hawatumii kadi hizo, napenda kusisitiza kuwa ifikapo tarehe mosi mwezi Machi mwaka huu tutasitisha kabisa matumizi ya tiketi za karatasi ili wasafari wote wanaotumia Mabasi ya Mwndokasi watumie kadi” Alisema Dkt.Kihamia

Alisema matumizi ya kadi yanaondoa usumbufu wa kukosekana kwa chenchi lakini pia ni njia muafaka ya kudhibiti uvujaji na upotevu wa mapato ya serikali.

Katika hatua nyingine Dkt.Kihamia alisema Serikali imeshaingia mkataba na mtoa huduma ya Mabasi ambaye atatoa huduma katika awamu ya pili ya mradi wa BRT katika Barabara ya Kilwa kuelekea Mbagala hivyo wananchi wa ukanda ho wakae mkao wa kula.

“Mambo ni mazuri sana Serikali sikivu ya Mh.Dkt.Samia Suluhu Hassan imeshafanya jambo lake kuanzia Machi 31 wakazi wa Mbagala na maeneo ya Jirani wataanza kufaidi huduma ya usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka maarufu kama Mwendokasi jambo ambalo wamelisubiri kwa muda mrefu” Alisema.

Aidha Dkt.Kihamia wakazi wa mbagala nao watatumia kadi janja pale huduma itakapoanza ili kuondoa changamoto za mfumo wa tiketi za karatasi kama zilizojiokeza katika awamu ya kwanza ya mradi.

Awali mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEI Mhandisi Gilbert Moga alisema mradi wa TOD japo umekamilika kwa kipindi cha miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake Serikali itaona namna ya kuuendelea kwani ni moja ya mambo ambayo yanaleta tija kubwa katika usafiri wa umma hasa kuleta maendeleo kwa wananchi wa pembezoni mwa mradi.

“Kukamilika kwa mradi huu ndio mwanzo wa sisi kama nchi kuona ni namna gani tunaendeleza maono haya ambayo wenzetu wa Japan kupitia JAICA kwa usimamizi wa DART wameanzisha kwenye TOD, niwahakikishie watanzania kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI itahakikisha mwendelezo wa mradi huu ili shoroba zote sita za mradi wa DART zinufaike na maendelezo haya ya TOD” Alisema.

Mradi wa TOD unahusisha kuboresha huduma za usafiri wa umma kwa kukusanya huduma za biashara,ofisi na makazi karibu na vituo vya usafiri, aidha unahusisha ujenzi wa maeneo rafiki ya waenda kwa miguu na kuboresha urahisi wa usafiri ili kuhamasisha matumizi ya usafiri wa umma.