Abiria wa Mabasi ya Yaendayo Haraka wapatiwa elimu ya TOD
Katika kutekeleza Mradi wa Maendeleo Yatokanayo na Maboresho ya Usafiri wa umma mijini (TOD), abiria wa Mabasi Yaendayo Haraka, leo Septemba 4, 2024 wamepata elimu kuhusu faida mbalimbali zitokanazo na uwepo wa mradi huo.
Elimu hiyo imetolewa na Maafisa wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) wakishirikiana na wataalamu wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi cha Gerezani.
Lengo kuu la elimu hiyo ni kujenga uelewa kwa abiria na wananchi kwa ujumla kuhusu maendeleo ya kijamii na kiuchumi ambayo yataletwa na maboresho kwenye usafiri wa umma ukimuwezesha abiria kusafiri kwa haraka sambamba na kupata huduma nyinginezo zinazopatikana karibu na miundombinu ya barabara na vituo vya Mabasi Yaendayo Haraka mfano masoko, makazi, ofisi, hoteli, shule, na vituo vya afya.