Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Sisi ni Nani?

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ni Wakala wa Serikali ulioanzishwa kwa Tangazo la Serikali Na. 120 la tarehe 25 Mei 2007 chini ya Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 ya mwaka 1997 pamoja na marekebisho yake. Kwa sasa, Wakala huu uko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI). DART ilianzishwa kwa lengo la kupanga, kuratibu na kusimamia utekelezaji wa mfumo wa kisasa wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) jijini Dar es Salaam.

Kuanzishwa kwa Wakala wa kulitokana na ukuaji wa kasi wa Jiji la Dar es Salaam uliosababisha msongamano mkubwa wa magari, changamoto za usafiri wa umma, kupotea kwa muda mwingi barabarani na athari za kimazingira. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliona umuhimu wa kuwa na mfumo endelevu, wenye ufanisi na uwezo mkubwa wa kubeba abiria ili kuboresha usafiri wa mijini na kuongeza tija ya kiuchumi.

Majukumu makuu ya Wakala wa DART ni kuanzisha, kudhibiti na kusimamia mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) unaojulikana kama Dar Rapid Transit (DART), kuhakikisha mtiririko mzuri wa magari katika barabara za mijini, pamoja na kusimamia kwa ufanisi miundombinu na huduma za mabasi yaendayo haraka. Wakala unasimamia ujenzi wa miundombinu, upangaji wa mfumo, uratibu wa wadau, udhibiti wa watoa huduma na uendeshaji wa mabasi katika njia maalum za DART.

Mradi wa DART unatekelezwa katika awamu sita kwa kuboresha miundombinu iliyopo kuwa njia maalum za mabasi. Hii inahusisha ujenzi wa njia maalum za mabasi, vituo vya kisasa na vituo vikuu, madaraja ya waenda kwa miguu, karakana pamoja na mifumo ya kisasa ya usimamizi wa usafiri ili kuhakikisha ufanisi, usalama na ubora wa huduma kwa viwango vya kimataifa.

Kwa sasa, Awamu ya Kwanza katika Barabara ya Morogoro yenye urefu wa kilomita 20.9 ipo katika uendeshaji na imeleta mageuzi makubwa katika usafiri wa umma jijini. Awamu ya Pili katika Barabara ya Kilwa yenye urefu wa kilomita 20.3 pia ipo katika uendeshaji na imepanua huduma za mabasi kwa maeneo mengi zaidi, hivyo kuimarisha muunganiko wa usafiri ndani ya jiji.

Awamu ya Tatu na ya Nne zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi kwa lengo la kupanua zaidi mtandao wa mabasi yaendayo haraka. Aidha, Awamu ya Tano na ya Sita zipo katika maandalizi ya kuanza ujenzi, jambo linaloonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha mfumo jumuishi wa usafiri wa umma jijini Dar es Salaam.

Mbali na ujenzi na usimamizi wa mfumo wa mabasi yaendayo haraka, Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka-DART unatekeleza pia mpango wa Maendeleo Yanayoongozwa na Usafiri wa Umma (Transit Oriented Development – TOD). Mpango huu unalenga kukuza maendeleo ya miji kuzunguka njia za BRT, kuboresha matumizi ya ardhi, kuchochea uwekezaji na shughuli za kiuchumi, na kujenga miji janja, endelevu na shirikishi kwa wakazi wa Dar es Salaam.