Ujumbe wa Mtendaji Mkuu
Karibu kwenye tovuti rasmi ya Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) ili kupata taarifa zaidi kuhusu utekelezaji wa mradi wa DART. Mradi wa DART ulifikiriwa kwanza mwaka 2002 na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na ukaingizwa katika mfumo wa usafiri wa jiji mwezi Aprili 2003 ili kukabiliana na changamoto za usafiri zilizokuwa zikiathiri wakazi wa jiji ambao walikuwa wakilitembelea maeneo tofauti kwa sababu mbalimbali. Moja ya changamoto zilizojitokeza na kuendelea kupunguza kasi ya maendeleo katika nyanja za kijamii na kiuchumi ilikuwa ni kuongezeka kwa msongamano wa magari ambao ulisababishwa na hali mbaya ya usafiri wa umma uliomilikiwa na watu binafsi mbalimbali pamoja na miundombinu ambayo haikuruhusu watumiaji wote wa barabara kufurahia usafiri wao wa kila siku.
Ili kufanya mradi kuwa endelevu, serikali ya Tanzania iliona kuwa ni muhimu kuanzisha Wakala ambao ungekuwa na jukumu la kusimamia mradi huo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wakati huo. Tangu serikali ya awamu ya tano ya Tanzania, Mradi wa DART unasimamiwa chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wakati huo. Uanzishwaji wa Wakala wa DART kupitia GN. 120 ya Mei 25, 2007 chini ya Sheria ya Wakala No. 30 ya 1997 na uzinduzi wake mnamo Juni 16, 2008 uliandaa hatua ya kuanza kwa Mradi wa DART ambao ulipangwa kutekelezwa katika awamu sita. Utekelezaji wa awamu hizo sita , umegawanyika katika makundi mawili makuu, ambayo ni, maendelezo ya miundombinu ya Mabasi yaendayo kwa Haraka (BRT) kwenye barabara kuu za jiji na usimamizi wa uendeshaji wa mabasi.
Awamu hizo sita ni pamoja na:
- Barabara ya Morogoro, Barabara ya Kawawa kaskazini, Mtaa wa Msimbazi, na Kivukoni Front— kilomita 20.9
- Barabara ya Kilwa, Barabara ya Kawawa Kusini— kilomita 20.3
- Barabara ya Uhuru, Barabara ya Nyerere, Barabara ya Bibi Titi, na Barabara ya Azikiwe— kilomita 24.3
- Barabara ya Bagamoyo, Barabara ya Sam Nujoma— kilomita 30.1
- Barabara ya Mandela, Barabara Mpya1— kilomita 27.6
- Barabara ya Mwai Kibaki— kilomita 26.5
Awamu zote sita za Mradi zinajumuisha kilomita 149.7
Utekelezaji wa Mradi wa DART awamu ya kwanza ulianza Agosti 2010 kwa maendelezo ya miundombinu ambapo ujenzi wake ulikamilika mwaka 2015. Maendeleo ya miundombinu ya DART yalijumuisha ujenzi wa barabara, vituo, na karakana. Vituo hivyo ni pamoja na Kivukoni ambacho kipo karibu na kivuko cha Kigamboni na soko la samaki, Kimara ambako ni mwisho wa ushoroba, na Kariakoo-Gerezani. Kituo kikuu kingine ni Morocco ambacho kipo mwisho wa kaskazini wa Barabara ya Kawawa. Kuna karakana mbili katika awamu ya kwanza, eneo la Jangwani na karakana ndogo mpya iliyojengwa karibu na kituo cha Ubungo.
Kwa kuwa ujenzi wa miundombinu ya mfumo wa DART Awamu ya Kwanza ulikamilika mapema zaidi kuliko ukamilishaji wa mchakato wa upatikanaji wa mtoa huduma, serikali iliamua kuanzisha oparesheni ya uendeshaji wa mabasi chini ya mtoa huduma wa mpito kama sehemu ya kulinda miundombinu mipya iliojengwa na kutumika kama fursa kwa serikali kujaribu ufanisi wa mfumo wa DART.
Ili kuwezesha watoa huduma za usafiri wa ndani kuendesha mfumo wa BRT, serikali ya Tanzania iliwaomba wamiliki wa mabasi ya abiria wa sasa kuunda kampuni ambayo ingeweza kufanya shughuli za uendeshaji wa mabasi kabla ya mtoa huduma kamili hajapatikana.
Tangu Mei 10, 2016, Wakala wa DART ulianza shughuli za uendeshaji wa mabasi kwa siku tano bila kuchaji abiria nauli ikiwa ni sehemu ya kuupa umma uzoefu wa mfumo mpya wa usafiri. Kuanzia Mei 16, 2016 hadi leo watumiaji hulipa nauli nafuu kati ya shilingi 750 kwa Njia Kuu na TZS 500 kwa Njia Mlishi. Katika Mfumo wa DART, kuna aina mbili za mabasi ambayo ni mabasi ya Njia Kuu na mabasi ya Mlishi. Basi refu linauwezo wa kubeba abiria wengi kama 120 kwa wakati mmoja huku basi Mlishi linauwezo wa kubeba abiria 50 hadi 60 kwa wakati mmoja.
Wakati wa mtoa huduma wa mpito, Wakala mnamo Agosti 2021 uliongeza mabasi 70 kwenye mfumo wa DART na kufanya jumla ya mabasi kuwa 210 kutoka 140. Kuongezeka kwa mabasi kumewezesha Wakala kuboresha huduma na kuunda njia mpya. Njia mpya ambazo zimeundwa ni pamoja na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli hadi Kituo Kikuu cha Kimara, Hospitali ya Mlongazila hadi Kimara, Kibaha hadi Kimara. Njia zingine ni Mbezi hadi Kivukoni, Mbezi hadi Gerezani Kariakoo.
Maendelezo ya miundombinu ya BRT inayoendelea ya Awamu ya Pili inahusisha kilomita 20.3 ikiwa na mafungu mawili ya ujenzi wa miundombinu, yaani, ujenzi wa barabara na ujenzi wa majengo. Katika Fungu la Pili linalohusika na ujenzi wa majengo, ilianza Mei 2019 na kukamilika Agosti 2021 huku fungu la kwanza linalohusika na ujenzi wa barabara ikiendelea kwa asilimia 29.43. Ujenzi wa barabara unataraji kukamilika kufikia Machi 2023.
Wakala umeanza ujenzi wa awamu ya Tatu ya Mradi inayohusisha kilomita 24.3 ikiwa ni pamoja na ujenzi wa njia maalum za mabasi yaendayo haraka, njia ya magari mchanganyiko, njia za watembea kwa miguu, vituo vikuu vitatu, vituo vidogo 32, karakana moja, na vituo mlishi vitatu. Aidha Wakala umeanza ujenzi wa awamu ya nne yenye urefu wa kilomita 30.1 katika barabara ya Al Hassan Mwinyi, Barabara ya Bagamoyo na Barabara ya Sam Nujoma, na ujenzi huo unafadhiliwa na Benki ya Dunia, ambayo pia ina fadhili awamu ya sita iliyoko kwenye kwenye hatua mbalimbali ya utekelezaji.
Kwa maranyingine tenaa tunakukaribisha kwenye mfumo wa DART kwa usafiri wa haraka mjini, wa kisasa na wa gharama nafuu.