Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
DART kusimika mfumo wa chaja za pikipiki zinazotumia umeme
23 Aug, 2024
DART kusimika mfumo wa chaja za pikipiki zinazotumia umeme

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) umesaini mkataba na Kampuni ya ZIOTIO-UN LTD itakayosimika mfumo wa Umeme katika miundombinu ya Mradi wa DART utakaotumika kuchaji Pikipiki za magurudumu matatu na zile za magurudumu mawili zinazotumia nishati hiyo kujiendesha.

Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo Agosti 22, 2024, Mratibu wa Mradi wa Solution Plus unaosimamia matumizi ya nishati salama katika usafirishaji, Bi. Delfina Mathias ambaye pia ni Meneja wa Mifumo ya Usafiri na Maendeleo ya Miundombinu ya DART, alisema mkataba huo ni juhudi za Wakala wa DART katika utunzaji wa mazingira.

 “Mradi huu ni mahsusi kwa ajili ya kutekeleza suala la last mile connectivity yaani mteja anapokuja kwenye miundombinu yetu ya DART kuchukua usafiri analetwa na nini na anaposhuka anapelekwaje kwake ambapo tulilenga zaidi katika teknolojia ya umeme tuweze kupambana na suala la uchafuzi wa mazingira”

Bi. Delfina amebainisha kuwa Wakala ulipata kampuni ambayo itaisaidia kuweka chaja za umeme kwa ajili ya kuchaji pikipiki na maguta na leo imekuja kusaini mkataba ili iweze kuleta chaja zitakazosimikwa kwenye miundombinu ya DART.

Amesema vituo kutakakofungwa chaja hizo ni pamoja na karakana ya Ubungo, Kituo Kikuu cha Gerezani na Morocco. Aidha, Wakala unataraji kuweka kituo kingine kwenye Kituo kikuu cha Mabasi cha Magufuli.

Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa Kampuni hiyo Bi. Mercy Kitomari amesema kuwa kazi ya kusimika chaja hizo itaanza ifikapo Septemba mosi mwaka 2024 ambapo kazi hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu.

“Tunatarajia kusimika charging stations kwa ajili ya wanaotumia guta, pikipiki na bajaji za umeme kuwa karibu yao ili kuwawezesha kuchaji vyombo vyao vya usafiri na kuendelea na biashara zao za usafirishaji wa mizigo na abiria” Amesema Bi. Mercy

Wakala wa DART kupitia Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka unatekeleza juhudi za utunzaji wa mazingira kwani kwa hivi sasa mabasi yake yanatumia teknolojia ya Euro III ambayo haizalishi hewa ukaa kwa kiasi kikubwa na katika mipango yake ijayo inataraji kuwa na mabasi yanayotumia gesi asilia pamoja na yale ya umeme ambayo hayachafui kabisa mazingira.