Wadau wa DART wakutana kujadili masuala ya uendeshaji
Wakati Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ikiendelea na mchakato wa Kumpata Mtoa huduma kutoka makampuni mbalimbali atakayeleta mabasi kwa ajili ya Awamu ya Kwanza ya katika Barabara ya Morogoro pamoja na Awamu ya Pili ya Barabara ya Kilwa, DART imekaa kikao na wadau wakuu akiwemo Mtoa Huduma ya Mpito ili kuboresha masuala ya uendeshaji.
Majadiliano hayo yamefanyika kutokana na kuwepo kwa malalamiko ya muda mrefu ya abiria kuhusu huduma isiyoridhisha inayohusianishwa na suala la uchache wa Mabasi kutoka Mtoa huduma.
Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa na wadau ni pamoja na kuondolewa kwa mageti janja yalisimikwa vituoni mwaka 2016 ikiwa sehemu ya njia ya ukusanyaji nauli ya Mtoa Huduma wa Mpito, njia inayotumika na DART kupima utendaji kazi na matokeo ya tozo kwa Mtoa Huduma ya Mpito kwenye shughuli za uendeshaji za kila siku.
Akifungua kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Wakala, Mtendaji Mkuu wa DART, Dkt. Athumani Kihamia, amesema majadiliano kuhusu masula ya uendeshaji yanapewa kipaumbele kwani kumekuwa na ufuatiliaji mdogo kwenye uendeshaji na hivyo kuzorotesha utoaji huduma bora kwenye mfumo wa DART.
“ Ningependa hata tuwe na vikao katika kila wiki ili tuweze kufikia matarajio ya abiria kila siku jijini. Sisi sote tunafanya kazi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani japo kwenye majukumu tofauti. Tufanye kazi kwa pamoja huku tukizungumza lugha moja kwa ajili ya wale tunaowahudumia.” Alisema Dkt. Kihamia.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa DART alipendekeza kuanzishwa kwa Kamati Maalum ikihusisha wajumbe kutoka DART ns Kampuni ya UDART ambayo Mtoa Huduma ya Mpito ya Mpito ili kufanya tathimini ya kuondosha mageti janja yaliyosimikwa awali na kusimika mageti janja mapya kwa ajili ya Mfumo wa Serikali wa Ukusanyaji Nauli – AFCS.
Dkt. Kihamia aliwaagiza wajumbe wa kikao kupendekeza adidu za rejea zitakazofanyiwa kazi siku chache kabla ya kikao kingine cha kujadili mapendekezo ya kamati.
Dkt. Kihamia pia aliuliza kuhusu muundo ambao umekuwa ukitumiwa na Idara ya Usimamizi na Uendeshaji wa Miundombinu ya Wakala wa DART katika kupima utendaji kazi kwa Mtoa Huduma ya Mabasi.
Kama njia ya kuendelea kupunguza gharama za uendeshaji, Dkt. Kihamia alipendekeza kuanzishwa kwa Kamati ambayo wajumbe wake watakuwa kutoka Idara ya TEHAMA na Fedha ya Wakala wa DART pamoja UDART ili kufuatilia kwa undani vigezo vipi vinaweza kutumika kumsimamia Mtoa Huduma wa Mpito ikiwa atashindwa kufikia vigezo vilivyowekwa kwenye mkataba kuzingatiwa baina ya pande zote mbili.
Akizungumzia suala la tozo kwa Mtoa Huduma ya Mpito, Mkurugenzi Mkuu wa UDART, Waziri Kindamba alipendekeza ulipaji kwa asilimia kwenda Serikalini kutoka kwenye makusanyo ya nauli kama ni muundo ulio sawa na hii ni kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji kila siku.
Akijibu ombi la ada ya uendeshaji kwa UDART, Dkt. Athumani Kihamia alipendekeza kuwe na majadiliano ya ndani kati ya DART na UDART ili kuondoa uzito wa baadhi ya mambo yanayoonekana kukwamisha utoaji huduma baina ya pande zote mbili.
Kikao hicho kilichodumu kwa takribani saa nne kilihudhuriwa ana Menejimenti ya Wakala wa DART, maafisa wa UDART, pamoja na Msajili wa Hazina ambaye pia ana hisa ya asilimia 85 katika kampuni ya UDART.