Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
DART yaungana na Wizara ya Afya kutoa Elimu kuhusu mlipuko wa Ugonjwa wa Homa ya Nyani
26 Aug, 2024
DART yaungana na Wizara ya Afya kutoa Elimu kuhusu mlipuko wa Ugonjwa wa Homa ya Nyani

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Leo Agosti 24,2024 umeungana na Wizara ya Afya kutoa elimu kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nyani maarufu kama MPOX kwenye kituo cha mabasi cha Mbezi Luis.

Elimu hiyo imeanza kutolewa mahsusi ikiwa ni kuupa umma uelewa mpana kuhusu athari za ugonjwa huo, dalili zake, namna unavyoambukizwa na jinsi ya kujikinga.

Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa DART, William Gatambi amesema kuwa Wakala pamoja na Wizara ya Afya wameungana kutoa elimu kuhusu ugonjwa wa MPOX unaoenea kwa kasi barani Afrika japo kwa Tanzania bado haijaripotiwa taarifa ya mgonjwa yeyote mpaka sasa.

“Kwa kuwa tuna wateja wengi kwenye vituo, tunashirikiana na Wizara ya Afya na jukumu letu ni kuwaelimisha abiria ili waweze kujikinga na ugonjwa huu na njia ambazo tutatumia kusambaza jumbe mbalimbali kuhusu ugonjwa huu ni pamoja na luninga, redio pamoja na mitandao ya kijamii pia tutaweka mabango kwenye vituo ili kutaadharisha” Alisema Gatambi

Gatambi amebainisha kuwa Wakala pia umejipanga kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na ugonjwa huu kama vile kuweka miundombinu ya kuwawezesha abiria na watumiaji wengine wa vituo kunawa mikono ambapo ametoa wito kwa umma kuzingatia kanuni za afya bora ili kujikinga na ugonjwa huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Kinga, Elimu ya Afya kwa umma kutoka Wizara ya Afya Dkt. Norman Kyala amesema mwitikio umekuwa mkubwa kama Wizara wanashukuru kwa kuweza kufikisha elimu na kuuhakikishia umma kuwa nchi iko salama kwani kwa sasa ugonjwa huu haujafika Tanzania.

“Wito wangu kwa abiria, madereva, watumiaji wengine wa vyombo vya usafiri na Watanzania kwa ujumla ni waendelee kufuatilia taarifa sahihi kuhusu ugonjwa wa MPOX kutoka kwenye vyanzo vya Wizara ya Afya, kufuatilia matangazo na vyombo vya habari vilevile kuzingatia kanuni bora za afya ili kujikinga” Amesema Dkt. Kyala

Miongoni mwa dalili kuu za ugonjwa wa MPOX ni homa, mapele yenye malengelenge na kuvimba mitoki na wataalam wa afya wanashauri jamii ikiwa uonapo dalili hizo ni vyema kuwahi kwenye vituo vya afya ili kuweza kupata msaada zaidi.