DART yakutana na wadau kujadili uvamizi katika barabara zake.
Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka-DART mapema mwezi Septemba umekutana na wadau mbalimbali wa usafiri wa umma katika mkoa wa Dar es Salaam, kujadili namna ya kutekeleza sheria sambamba na kuona namna bora ya matumizi sahihi ya vyombo vya moto vinavyotakiwa kupita katika barabara za Mabasi Yaendayo Haraka.
Mkutano huo wa wadau uliofanyika katika Shule ya Sheria kwa vitendo ambao ulikua chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Heri James, uliitishwa na DART kwa lengo la kuwekeana mikakati na uelewa wa pamoja wa namna ya kutumia miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka baada ya DART kuanza operesheni ya kuzuia magari binafsi na ya watu binafsi yanayovamia na kupita barabara hizo.
Operesheni hiyo ambayo imekuja kutokana na kukithiri kwa watumiaji wa barabara hizo ambao kisheria hawatakiwi kutumia barabara za Mabasi Yaendayo Haraka, kuliibua sintofahamu kwa baadhi ya mamlaka kutoheshimu utaratibu ambao unatakiwa kufuatwa wa namna ya kutumia miundombinu hiyo.
Akizungumza katika mkutano huo mkuu wa Wilaya ya Ubungo ambaye alikua mwenyekiti, alitaka zoezi hilo kuendeshwa kwa staha na kwa kuzingatia aina ya dharura ambayo inaweza kupelekea aina fulani ya magari binafsi na hata ya serikali kupita katika barabara za mwendokasi.
“Kuvunja sheria kwa mtu yoyote yule ni kosa , hata sisi viongozi hatuko juu ya sheria, rai yangu leo kwa kuwa tumekutana hapa kujadili namna bora ya kuendesha zoezi hili, ni vyema tukaja na mkakati ambao hautaathiri utendaji kazi wa taasisi ama mamlaka nyingine,”alisema.
Nawasihi sana DART zoezi ni jema sana lakini wakati linatekelezwa lisije kuleta madhara, mfano kuna mgonjwa mahututi anatakiwa kuwahishwa hospitali ili kuoka maisha yake katika hali hii busara itumike ili raia mwenzetu huyu asipoteze maisha, alisema.
Mkutano huo ambao uliwahusisha wakuu wa wilaya za mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha ulijadili mikakati ya kupunguza uvamizi wa miundombinu na barabara za Mabasi Yaendayo Haraka, pia ulisisitiza umuhimu wa viongozi kutii sheria na kama kutakuwa na ulazima ama dharura ambayo italazimu chombo cha moto kupita katika barabara za mwendokasi, mawasiliano yafanyike mapema na DART ili kuruhusu matumizi ya njia hizo kwa wakati husika.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam William Mkonda alisisitiza kuwa suala la kwenda kazini sio dharura hivyo atawashangaa sana maafisa wa jeshi hilo ambao hawatakuwa na dharura wala kazi maalum wakipita katika barabara za Mabasi Yaendayo Haraka.
“Ndugu zangu niweke wazi kabisa hata Afande IJP Wambura alishalitolea ufafanuzi suala hili kwenda kazini sio dharura, wewe kama kiongozi unatakiwa uwahi kuamka ili ukatekeleze shughuli zako kama muda wako wa kazi unavyokuhitaji, haiwezekani umechelewa kuamka unajiamulia kuingia kwenye barabara za Mwendokasi kisa wewe ni askari hii sio sawa” Alisema Kamishna Mkonda.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni ACP Mtatiro Kitinkwi alisema suala la utii wa sheria haliangalii wadhifa wa mtu, ni vyema viongozi kutii sheria ili wananchi nao waige mfano bora wa viongozi wanaofuata sheria.
Alisema katika mkoa wakipolisi wa Kinondoni watahakikisha wanashirikiana na DART kudhibiti wavamizi wote wanaoingilia barabara za Mabasi Yaendayo Haraka ili umuhimu na upekee wa mradi huo uendelee kuwepo kwa manufaa ya wananchi.
“Mimi ni muumini wa kufuata sheria kanuni na taratibu, hivyo niwahakikishie DART ushirikiano mkubwa wa kulinda miundombinu hii isitumike vibaya na kwa maslahi ya wachache”, alisema ACP Kitinkwi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa DART, Dr.Edwin Mhede aliwaambia wajumbe kuwa Wakala umeamua kukaa pamoja na wadau wa usafiri wa umma ili kuona athari za wanaovamia miundombinu ya BRT ikiwemo ajali zinazosababishwa na magari yanayoingilia mfumo huo.
Alisema kwa siku moja pekee katika kipindi cha nyuma zaidi ya magari 250 hadi 300 yalikua yanapita katika barabara za mabasi, jambo ambalo linasababisha usumbufu kwa watumiaji wa mabasi hayo.
“Niwaambie tu ndugu zangu sisi tuna mabasi 200 hadi 210, sasa na magari mengine 300 yakichangayika kwenye barabara hizo hizo maana ya usafiri wa haraka itakuwepo?, tujiulize tu miundombinu hii ambayo lengo lake ni kuwapunguzia adha wana Dar es Salaam kama tunaitendea haki,” alisema Dr.Mhede.
Kikao hicho cha wadau mbali na kuhudhuriwa na wakuu wa Wilaya za mkoa wa Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, kiliwahusisha pia wadau wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka kama LARTA, UDART, kampuni ya usafi ya Moma, pamoja na Kampuni ya Ulinzi ya China Security.
Aidha, Maafisa waandamizi wa Jeshi la Polisi walihudhuria pia kikao hicho akiwemo ACP Debora Magiligimba, ACP Mtatiro Kitinkwi, ACP William Mkonda, ACP Kennedy Mgani, Pamoja na ACP Gerard Ngichi.