DART yatangaza ofa kwa wanunuaji kadi
Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) umetangaza ofa kwa abiria watakaonunua kadi za Mwendokasi ikiwa ni ofa maalum kuelekea msimu wa Sikukuu za mwisho wa mwaka.
Ofa hiyo imetolewa leo Novemba 22,2024 na Mtendaji Mkuu wa DART, Dkt. Athumani Kihamia wakati wa Mkutano wake na Waandishi wa Habari Ubungo Maji Dar es Salaam.
Dkt. Kihamia amesema kuwa ofa hiyo mahususi ni kwa wateja wote ambao watanunua kadi hiyo kwa shilingi 5000 ikiwa ndani yake na kiasi cha shilingi 3000.
Aidha Dkt. Kihamia amesema kuwa ofa hiyo ni maalum kwa ajili ya kuhamasisha matumizi ya Kadi Janja kwenye Mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka na kutokomeza matumizi ya tiketi za karatasi.
Dkt. Kihamia ameongeza kuwa matumizi ya kadi janja kwenye kulipa nauli ni mfumo salama wa ukusanyaji wa fedha za serikali.
Ofa hiyo imekuja ikiwa imepita miezi miwili toka kuzinduliwa kwa Kadi hizo Septemba 2,2024 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- TAMISEMI Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa.
Kadi za Mwendokasi zinatumika kwenye Njia Kuu ya Kimara hadi Kivukoni na Matawi ya Fire mpaka Gerezani na Magomeni mpaka Morocco. Vilevile kadi hizo zinatumika kwenye Njia Mlishi kutoka Kimara mpaka Mbezi Luis na Kituo cha Mabasi cha Magufuli.