DART yatangaza vituo mbadala vya daladala katika Kituo Kikuu cha Kivukoni
Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Oktoba 9,2023 wametangaza njia na vituo mbadala vitakavyotumika kupakia na kushusha abiria wa usafiri wa Daladala eneo la Kivukoni kwa kipindi chote cha ujenzi wa Miundombinu ya Mradi wa DART Awamu ya Nne kuelekea Tegeta.
Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano DART, Bw. William Gatambi amesema wakati sasa umefika wa utekelezaji wa ujenzi wa Mradi wa DART Awamu Nne hivyo amewaomba watumiaji wote wa kituo cha Kivukoni kupisha eneo hilo ili kumpa Mkandarasi nafasi ya kutosha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa mradi huo kwa wakati.
Aidha, Bw. Gatambi amewataka wananchi kutoka maeneo mbalimbali waliokuwa wakitumia Kituo hicho kuwa wavumilivu kwa kipindi chote ambacho watakuwa wanatumia barabara na vituo mbadala vilivyoainishwa mpaka pale ujenzi utakapokamilika.
Bw. Gatambi amebainisha vituo vilivyoainishwa ni pamoja na eneo karibu na Wizara ya Ardhi kwa watumiaji wa daladala wanaoelekea Kigogo Sokoni, Tabata Chang’ombe, Kinyerezi, Machinga Complex na Buyuni Sokoni kupitia Barabara ya Nyerere, Uhuru, Machinjioni, Mnyamani na Bibi Titi.
Vituo vingine ni pamoja na eneo karibu na Benki ya NBC (Posta ya Zamani) kwa wanaoelekea Kisemvule, Kivule Sokoni, Mbande Kisewe, kupitia Barabara ya Kilwa, Nyerere na Uhuru. Na Kituo cha Mwisho ni eneo lililopo kwenye Mtaa wa Ohio kwa wanaoelekea Gongolamboto na Tegeta Nyuki kupitia Barabara ya Nyerere, Uhuru na Ali Hassan Mwinyi.
Mabadiliko haya yanayotaraji kuanza kutekelezwa tarehe 21 Oktoba 2023, yanakuja wakati ambapo Mkandarasi akiwa kwenye hatua za mwisho za maandalizi ya upanuzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi Yaendayo Haraka cha Kivukoni kinachotumiwa na Abiria Awamu ya Kwanza kuelekea Kimara na ambacho kitatumika na abiria wa Awamu ya Pili kuelekea Mbagala, Awamu ya Tatu kuelekea Gongolamboto na Awamu ya Nne.
Maamuzi hayo yamefikiwa baada vikao vya pamoja kati ya DART na Wadau wengine wa usafiri wa umma akiwemo, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Halmashauri ya Jiji, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA), Chama na Umoja wa Wamiliki wa Daladala (DARCOBOA na UWADAR).
Ujenzi wa miundombinu ya Mradi wa DART Awamu ya Nne unataraji kukamilika ndani ya miezi 18 ambapo kwa Miundombinu ya Kituo Kikuu cha Kivukoni itakamilika ifikapo mwezi Oktoba 2024.