Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
E - Wallet yaongezwa kwenye Mwendokasi APP
12 Aug, 2024
E - Wallet yaongezwa kwenye Mwendokasi APP

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka - DART umefanya maboresho kwenye programu tumizi ya kununulia tiketi za safari maarufu Mwendokasi App kwa kuongeza E- Wallet ili kurahisisha zaidi matumizi ya programu hiyo.

 

Tofauti na zamani, kwa kutumia E-Wallet, sasa mtumiaji atanunua tiketi moja kwa moja, badala ya kupitia kwanza katika mitandao ya simu.

 

Ili kuweza kutumia huduma hii mpya, abiria atapaswa kuipakua mwendokasi App katika simu janja yake yenye mfumo android au IOS ambako ndani yake ndiko inakopatikana E- Wallet.

 

Aidha kwa wale abiria ambao tayari walishaipakua Mwendokasi App hapo awali, watatakiwa kuihuhisha (Update) ili kupata maboresho hayo yenye E- Wallet.

 

Akielezea kuhusu E- Wallet, Kaimu Meneja wa Mifumo na Miundombinu ya TEHAMA wa DART, Bi. Mariam Lusewa alisema, E- Wallet ni akaunti inayotumika kuhifadhia fedha ambazo hutumika kununulia tiketi za Mabasi Yaendayo Haraka.

 

Bi. Lusewa ametaja faida za kutumia E-Wallet kuwa ni pamoja na kumsaidia abiria kudhibiti fedha zake kwa kuweka bajeti ambapo inakuwa rahisi kwake kuwa na uhakika wa kupata tiketi kwa muda aliojiwekea.

 

Faida nyingine alisema E-Wallet itamsaidia abiria kupata tiketi kwa haraka zaidi na muda mwingine kumuepusha kuchelewa kwa kusubiria chenji pale anaponunua tiketi dirishani.

 

Huduma hii ya E- Wallet ni muendelezo wa DART kutoa huduma kidigital ili kuwafanya abiria wake kufurahia huduma za usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka.