Kamati ya Bunge ya TAMISEMI yaridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa miundombinu Mradi wa DART Awamu ya Tatu
Kamati ya Bunge TAMISEMI yaridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya DART Awamu ya Tatu.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Miko na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeridhishwa na Maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka DART Awamu ya Tatu unaotekelezwa kuanzia katikati ya Jiji hadi Gongolamboto kupitia Barabara ya Nyerere.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi katika mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mh.Denis Londo (Mb) alisema, kasi ya ujenzi wa miundombinu inaridhisha na akawataka Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka kuzidi kuimarisha usimamizi ili mradi huo ukamilike kwa wakati na katika ubora unaohitajika.
“Nimeshuhudia namna mkandarasi anavyoendelea na kazi, nitoe rai kwa DART kuhakiklisha kazi inakamilika kwa mujibu wa muda uliopangwa katika mkataba na pia kuhakikisha kuna kuwa na ubora wa kazi unaolingana na thamani ya fedha iliyotumika” Alisema.
Aidha Mwenyekiti huyo wa Kamati alisisitiza umuhimu wa wazawa kushirikishwa katika ujenzi wa miradi mikubwa na ya kimkakati kama huo ili mradi unapokamilika ujuzi walioupata uweze kutumika katika kuendeleza miradi mingine hata pale wataalam wa nje wanapokuwa wameondoka.
“Kamati inaelekeza pia Wakala kwa kushirikiana na Wizara kuona namna wazawa wanaofanya kazi katika mradi huu wanaendelea kutumia ujuzi walioupata ili kwenda kusaidia katika ujenzi wa miundombinu mingine hapa nchini” Mhe. Londo alisema.
Kwa upande wake Wazizi wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mh.Angelah Kairuki (Mb) alisema Wizara yake itahakikisha miradi yote iliyoko chini yake inakuwa na ubora na viwango vya kimataifa ili thamani ya fedha iliyotumika iendane na ubora wa kazi iliyofanyika.
“Naomba niihakikishie kamati kuwa miradi yote iliyoko chini ya TAMISEMI tutahakikisha inakuwa na ubora na pia inakamilika kwa wakati kwa mujibu wa mikataba ili tuendelee kumpa nguvu Rais wetu Mh. Dkt Samia Suluhu Hassan katika mageuzi makubwa anayofanya katika kuendeleza sekta mbali mbali za kiuchumi hapa nchini” Alisema Waziri Kairuki.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa DART, Mhandisi Fanuel Kalugendo alisema Barabara ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka awamu ya tatu ina jumla ya kilomita 23.6 ambayo imegawanywa katika mafungu mawili ambapo kipande cha kwanza kinafanywa na mkandarasi Sino Hydro kutoka China na kipande cha pili kwa upande wa ujenzi ambacho kiko kwenye hatua za mwisho za usanifu kiko chini ya kampuni ya UNITEC Civil Consultant ya Tanzania.
Aidha Mhandisi Kalugendo aliiambia kamati kuwa,DART inaendelea na usanifu na usimamizi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka ambayo kwa Jiji la Dar es Salaam imegawanyika katika awamu sita ambapo zikikamilika usafiri katika mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya Jirani utakua umerahisishwa na kuimarika na hivyo kukuza uchumi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa DART, Dkt. Florens Turuka aliishukuru kamati ya Bunge kutembelea Wakala na kuahidi kuendelea kusimamia na kushauri ipasavyo katika masuala yote yanayohusu maendeleo ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka.
Pia alisisitiza kuwa DART inaendelea na mchakato wa kuhakikisha mabadiliko ya Sheria yanakamilishwa ili Wakala uweze kupewa mamlaka ya kuendeleza miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka nchi nzima.