Kamati ya Bunge yaipa Kongole DART
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) Mh.Jerry Silaa amesema kamati yake imeridhishwa na utendaji kazi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), na kushauri Wakala huo kupanua wigo wa usanifu wa barabara zake ili kuendana na mahitaji ya sasa kwani ukuaji wa makazi na maendeleo katika Mkoa wa Dar es Salaam unakwenda kwa kasi..
Akizungumza wakati ziara ya Kamati hiyo kwa DART Septemba 3, 2022, Mh.Jerry Silaa alisema kuna umuhimu na ulazima kwa Wakala kujiongeza na kufikiria kupanua wigo wa miundombinu yake ili iweze kuwafikia watu wengi zaidi ikizingatiwa kuwa upembuzi unaotumika kwa sasa ni ule ambao ulifanyika miaka ya 2003 na 2004 kipindi ambacho idadi ya wakazi wa Dar es Salaam haikuwa kubwa.
“Nichukue fursa hii kuwapongeza kwa dhati kabisa DART, mnafanya kazi nzuri sana ya kuwahudumia wakazi wa Dar es Salaam, lakini bado kuna uhitaji mkubwa wa kupanua huduma zenu kwani maendeleo yanakimbia sana, mjitahidi kuendana na wakati, kama mlifikiria kuishia katika awamu sita tu mjipange kuona uwezekano wa kujitanua zaidi na zaidi kwani kasi ya kukua kwa miji inaenda mbio sana, ” alisema Silaa.
Alisema, “Wakala ufikirie kupangua na kurekebisha michoro yake ili kuwafikia watu wengi zaidi, mfano wa barabara inayotakiwa kuishia Boko DAWASA iende hadi Mapinga mpakani mwa Dar es Salaam na mkoa wa Pwani, pia kwa upande wa barabara ya Kilwa msiishie tu vikindu muone namna hata ya kusogea mbele zaidi, kadhalika mradi wa awamu ya tatu kuelekea Pugu usogee nao hadi Chanika ikiwezekana mfike mpaka Kisarawe.”
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka, Dr. Edwin Mhede, aliiambia kamati kuwa lengo la Wakala ni kuongeza wigo wa huduma zake ili kuiyafikia maeneo mengi ya mkoa wa Dar es Salaam na majirani zake, lakini pia baadaye wanafikiria kupeleka BRT kwenye miji mikubwa na yenye shughuli nyingi kiuchumi kama Arusha, Mbeya, Mwanza, na Makao Makuu ya nchi Dodoma.
Aidha, alisema Wakala utaendelea kujiimarisha kimifumo hasa katika maeneo ya Tehama ili kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato kwa kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato baada ya kuanza kutumika kwa mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa nauli wa AFCS.
“Waheshimiwa wajumbe, mkakati huu wa kutumia AFSC umetuwezesha kuvuka malengo tuliyojiwekea ya ukusanyaji wa mapato, hata hivyo tunaendelea kukamilisha hatua za ununuzi wa mageti pamoja na kukamilisha miundombinu ya matumizi ya kadi ili kila msafiri aanze kutumia kadi kama ilivyokuwa awali”, alisema Dr. Mhede.
Mjumbe wa Kamati hiyo na aliyekua Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa, alisema kuwa tayari hatua zimeshachukuliwa kuiwezesha DART kimuundo ili iweze kutekeleza majukumu yake kama lengo la kuanzishwa kwake linavyosisitiza.
Kuridhiwa kwa muundo mpya wa Wakala kutaongeza ufanisi na ari ya utekelezaji wa majukumu, hivyo kurahisisha utoaji wa usafiri wa umma wa uhakika na wa kutegemewa zaidi katika mkoa wa Dar es Salaam.
Sambamba na kuridhiwa kwa muundo mpya wa Wakala Serikali pia ipo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba wa kuleta mabasi mapya 177 ambayo kwa kiasi kikubwa yakiingia katika mfumo yataondoa tatizo la uhaba wa mabasi.
Kamati ya PIC ilipata fursa ya kukagua na kutembelea mradi wa DART katika vituo vya Kimara ,Gerezani, na kituo kikuu cha Mbagala Rangitatu ambacho kimekamilika kwa asilimia mia moja.
Awamu ya kwanza ya mtandao wa barabara za DART yenye urefu wa kilometa 20.9 inahusisha barabara za Morogoro kuanzia Kimara hadi Kivukoni, Pamoja na matawi yake katika barabara ya Kawawa eneo la Magomeni hadi Morocco , eneo la Msimbazi Fire hadi Gerezani Kariakoo.
Nyingine ni awamu ya pili inayohusisha barabara ya Kilwa kuanzi Gerezani hadi Mbagala Rangitatu, na awamu ya tatu inayohusisha barabara ya Nyerere kuanzia katikati ya mji hadi Gongolamboto, awamu ya nne itazihusisha barabara za Sam Nujoma na Ali Hassan Mwinyi.
Mtandao wa barabara hizo pia utazihusisha barabara za Nelson Mandela Pamoja na ile ya Tabata dampo hadi Segerea ambazo ni awamu ya tano, vilevile kutakuwa na awamu ya sita katika barabara ya Mwai Kibaki na nyongeza za Kimara hadi Kibaha Pamoja na Mbagala Rangitatu hadi Vikindu.
Mwisho