Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Mkurugenzi ataka kuwekwa vipaumbele katika bajeti
06 Feb, 2024
Mkurugenzi ataka kuwekwa vipaumbele katika bajeti

Wakati Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka -DART inaendelea na usimamizi wa huduma ya usafiri wa umma jijini Dar es Salaam, maafisa wa wanaoshughulika na uandaaji wa bajeti kutoka kila idara na vitengo wametakiwa kuzingatia vipaumbele vilivyoainishwa na Serikali, sambamba na kufuata miongozo na kanuni zinazosimamia fedha za umma kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Fedha wa Wakala, CPA.Casmir Deusdelity alipokuwa akitoa mwelekeo wa uandaaji za serikali kwa maafisa bajeti wa DART katika ufunguzi wa  kikao kazi cha maandalizi ya bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 ambacho kimefanyika hivi karibuni mjini Kibaha.

 “Nawasihi maafisa bajeti wote kufanya bajeti, kulingana na vipaumbele vya Wakala na miongozo iliyotolewa na Serikali ikiwemo Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti 2024/2025 na maelekezo kutoka ofisi ya Msajili wa Hazina na kutumia maoteo ambayo kila idara na kitengo iliwasilisha.” amesema CPA Casmir.      

 Mkurugenzi huyo wa fedha amesistiza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza vipaumbele vyake ilivyojiwekea katika dira ya maendeleo ya Taifa inayotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ambayo ilianza kutekelezwa tangu mwaka 2021 na inatarajia kukamilika mwaka 2026.

Aidha, alisema, uandaaji wa bajeti za Serikali una vipaumbele vilivyoainishwa kama vile mipango ya maendeleo ya muda mfupi, wa kati, na muda mrefu ambavyo vyote ni lazima kuwekewa mkazo wakati wa uandaaji wa bajeti.

Vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Taifa wa Maendeleo viko katika maeneo matano ambayo ni pamoja na kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimaisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, kukuza uwekezaji na biashara, kuchochea maendeleo ya watu, na kuendeleza rasilimali watu.

Akizungumzia suala la makusanyo ya utoaji wa huduma katika vituo, CPA Casmir amesema kuwa Wakala unaendelea kuboresha mazingira ya utoaji huduma ili kuweza kuongeza mapato ya Wakala kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ikiwa ni pamoja na kuongeza mabasi na kufunga mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji nauli.

Pia, amewataka maafisa bajeti kufanya kazi kwa weledi na kujituma ili kuandaa bajeti yenye viwango na itakayokubalika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pale itakapowasilishwa.

Kadhalika amewaasa maafisa bajeti kuandaa bajeti zao kulingana na muundo mpya wa DART.

Kazi ya uandaaji bajeti ya DART imefanyika Februari mwaka huu kwa ushirikiano na Maafisa Mipango kutoka kitengo cha Mipango na Tafiti serikalini   ili iunganishwe na bajeti ya taasisi za TAMISEMI kabla ya  kupelekwa bungeni kwa ajili ya kusoma na kupitishwa.