Madiwani Manispaa ya Ubungo wapitisha ujenzi wa Karakana eneo la Simu 2000
Baraza la Madiwani la Manispaa ya Ubungo leo Julai 4, 2024 limepitisha ujenzi wa karakana ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Nne inayotarajiwa kujengwa eneo la Simu 2000 katika Manispaa hiyo.
Maamuzi hayo yamefikiwa katika kikao cha baraza hilo lililohudhuriwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ubungo pamoja na DART kama wageni waalikwa.
Lengo la kikao hicho ilikuwa ni kuwapa uelewa wa kina kuhusu Mradi wa DART Awamu ya Nne na hatimaye watoe maamuzi yatakayopelekea kukamilisha kwa wakati utekelezaji wa ujenzi huo.
Akichangia katika kikao hicho, Diwani wa Kata ya Goba, Mhe. Ester Ndoha ameupongeza Wakala wa DART kwa kuja na mpango huo wa kimkakati kwa ajili ya manispaa hiyo.
“Naomba niseme tu ombi kwa ajili ya ujenzi wa karakana kwenye eneo hilo limepitishwa na iwape pongezi kubwa wenzetu wa DART kwa kuja na mpango mkakati mahsusi, mradi huu sio tu utaleta fedha pia utaongeza chachu ya maendeleo kwenye manispaa yetu” Amesema Mheshimiwa Ndoha.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mheshimiwa Hassan Bomboko alipopewa nafasi kutoa salam, amemshukuru Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mheshimiwa Jaffary Nyaigesha kupitia Baraza hilo kwa kukubali ombi la DART kuchukua na kuanza utekelezaji wa ujenzi wa karakana hiyo kwa wakati na kuongeza kuwa maendeleo yoyote lazima yaje na mabadiliko hivyo wananchi wawe wavumilivu kwa muda.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Usafirishaji wa Wakala wa DART, Mhandisi Mohamed Kuganda akiwasilisha taarifa ya ujenzi huo, amesema kuwa Wakala wa DART umepanga kujenga karakana hiyo ikiwa ni mkakati mahsusi kukamilisha Awamu ya Nne ya Mradi wa DART na kuwa karakana hiyo itajengwa sambamba na karakana nyingine iliyoko eneo la Mbuyuni (Njia panda ya Kunduchi) ambapo Mkandarasi anasubiri kukabidhiwa eneo ili aanze rasmi ujenzi.
Mhandisi Kuganda ameongeza kuwa kabla ya ujenzi kuanza wadau wa usafirishaji pamoja na wafanyabiashara watatengewa eneo ili shughuli zao ziweze kuendelea kama kawaida na amelihakikishia Baraza hilo kuwa hakuna yeyote ambaye atapisha ujenzi pasi na kupewa eneo mbadala.