Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Mkurugenzi Mkuu TAESA aipongeza DART kwa malezi mazuri kwa Watumishi Tarajali
22 Sep, 2023
Mkurugenzi Mkuu TAESA aipongeza DART kwa malezi mazuri kwa Watumishi Tarajali

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) umepongezwa kwa malezi mazuri wanayowapa Watumishi Tarajali wanaofanya kazi katika Wakala huo.

Pongezi hizo zimetolewa leo Septemba 22,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA), Bw. Joseph Nganga wakati wa kikao kazi kilichojumuisha DART, TaESA na Viongozi wa Watumishi hao.

Mkurugenzi Nganga amesema Wakala wa DART umekuwa ni mfano wa kuigwa na Taasisi nyingine kwani mbali na kuwapatia nauli, pia wameweza kuwapatia watumishi hao Bima ya Afya ya NHIF na kuwawekea akiba katika mfuko wa hifadhi ya jamii wa PSSSF hali inayoongeza motisha kwa vijana hao kufanya kazi kwa bidii na uaminifu mkubwa na hivyo kuongeza tija kwa Taasisi na Taifa kwa ujumla.

“Nilifikiri majaabu hayapo duniani ila leo nimeyaona. DART ni taasisi ya kwanza kuwapatia watumishi Tarajali Bima za Afya na kuwawekea akiba katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii” amesema Bw. Nganga.

Aidha amewaasa watumishi hao kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia weledi wa kazi, maadili, mtazamo chanya, ubunifu na mawasiliano mazuri baina yao na Viongozi wa DART wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwani ndiyo nguzo imara katika Utumishi wa Umma.

“Nawaomba muwashangaze DART. Ninaposema ishangazeni DART namaanisha kuishangaza katika kutimiza malengo yake kwa kufanya kazi kwa bidii na kuwa wabunifu.” Alisema Bw. Nganga.

Bw. Nganga pia alitumia fursa hiyo kuwakaribisha watumishi hao Tarajali kutoa maoni na michango ya kuboresha taasisi hiyo pale watakapoona inafaa.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka(DART), Dr. Edwin Mhede ameishukuru TaESA kwa kuwapatia vijana hao kwani wamekuwa msaada mkubwa kwa Wakala katika kutimiza malengo yake.

Dr. Mhede amemuhakikishia Mkurugenzi Mkuu wa TaESA kwamba vijana hao wako kwenye mikono salama na ni ukweli usiopingika kwamba hajasikia sifa mbaya zinazoharibu utumishi wa umma.

“Nitakuwa mtu wa ajabu kuona vijana mlionipa niwalee wanaharibikia mikononi mwangu” alisema Dr. Mhede. “Nashukuru sijasikia matukio ya ulevi kuwahusu wao na vilevile sijasikia tabia za uzinzi.”

Aidha Dr. Mhede amesema mbali na mafunzo mbalimbali wanayowapatia mara kwa mara kama mwongozo katika utendaji kazi wao, Wakala wa DART pia umetoa fursa ya watumishi hao kumiliki viwanja katika jiji la Dodoma ambavyo wanalipia kidogo kidogo.

Vilevile Dr. Mhede amemuhakikishia Mkurugenzi Mkuu wa TaESA kuwa Wakala wa DART utaendelea kuwahitaji vijana hao kwani kufikia mwaka 2024, huduma ya usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka itakuwa imeenea sehemu kubwa ya Dar es salaam na hivyo kuhitaji nguvu kazi yao.

Naye Kiongozi wa Watumishi hao Bw. Paxley Mwenitete mbali na kuomba kuongezewa muda wa kuhudumu DART, aliishukuru TAESA kwa kuwapa fursa ya kufanya kazi na Wakala wa DART kwani Wakala huo kupitia Mtendaji Mkuu wamefundishwa kazi na kupatiwa malezi bora yatakayowasaidia kimaisha.

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka ina Watumishi Tarajali 100 wanaohudumu katika Mradi wa DART katika vitengo mbalimbali ambao hupatikana kupitia Wakala wa Huduma za Ajira.