Naibu Waziri TAMISEMI aipongeza DART kwa mageuzi makubwa kiutendaji
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mh. Zainab Katimba ameupongeza Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART kwa mageuzi makubwa ya kiutendaji hasa kuanza kwa matumizi ya mageti na kadi janja.
Akizungumza katika Ofisi za Wakala Ubungo Maji Jijini Dar es Salaam alipofanya ziara ya kikazi, Mh. Katimba alisema TAMISEMI ina imani kubwa na kazi inayofanyika hivyo akasisitiza watumishi kutobweteka badala yake waongeze bidii zaidi katika utendaji kazi
“Napenda nitoe pongezi zangu za dhati kwa jitihada zinazofanywa na DART hasa kuanza kutumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya nauli, jitihada hizi zinaenda kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kuimarisha makusanyo” Alisema Naibu Waziri.
Aidha Mh. Katimba ameupongeza Wakala kwa ukamilishaji na uendelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya Mradi akitoa mfano wa ujenzi wa miundombinu ya Awamu ya Pili kuelekea Mbagala, Awamu ya tatu ya ujenzi wa miundombinu kuelekea Gongolamboto pamoja na awamu ya Nne kuelekea Tegeta.
Akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Wakala, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa DART, Dkt. Athuman Kihamia amesema kwa sasa huduma inaendelea kutolewa kwenye Awamu ya kwanza ya Mradi kutokea Kimara hadi Kivukoni, Kimara hadi Gerezani na Kimara hadi Morocco pamoja na kwenye njia mlishi.
Aidha Dkt. Kihamia amesema kuwa ujenzi wa miundombinu kwenye Awamu ya Pili ya Mradi umekamilika kwa asilimia 99 ambapo hatua zinazoendelea kwa sasa ni za kumnunua mtoa huduma ya Mabasi kwenye awamu hiyo ili huduma ya usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka iweze kuanza.
Vilevile Dkt. Kihamia amebainisha kuwa ujenzi wa miundombinu ya Awamu ya Tatu na ile ya Nne inaendelea kwa kasi kubwa na mikakati iliyopo katika Wakala ni kuhakikisha kuwa miundombinu ikikamilika na watoa huduma wanapatikana.
Aidha Dkt.Kihamia amebainisha kuwa mchakato wa kumpata mtoa huduma wa kudumu katika awamu ya kwanza uko katika hatua nzuri na inatarajiwa hivi karibuni mkataba utasainiwa mara baada ya taratibu za kiuwekezaji kukamilika.