Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Ninahitaji ushirikiano DART - Dkt Kihamia
16 Jan, 2024
Ninahitaji ushirikiano DART - Dkt Kihamia

Mtendaji Mkuu mpya wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Dkt. Athuman Kihamia ameisihi Menejimenti ya Wakala wa DART kuwa na ushirikiano naye wakati wa utekelezaji wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka uliopangwa kutekelezwa katika awamu sita. 

Dkt. Kihamia amesema hayo Januari 16, 2024  wakati wa makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa DART, Dkt. Edwin Mhede jijini Dar es Salaam.  

Makabidhiano hayo yameshuhudiwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Rogatus Mativila, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala Prof. Florens Turuka, Mwenyekiti wa Bodi ya ukaguzi ya DART, CPA Jamhuri Ngelime pamoja na Menejimenti ya DART.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Kihamia ameshukuru kwa mapokezi mazuri aliyoyapata na ameahidi ushirikiano wa kutosha kwa Menejimenti na watumishi wa Wakala.

“Katika kutekeleza majukumu ya umma hakuna miujiza bali ni kwa watumishi kila mmoja kwa nafasi yake kujituma na kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano” Alisema Dkt. Kihamia.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa awali Dkt. Edwin Mhede alimueleza Dkt Kihamia kuwa Wakala wa DART uko na watumishi wenye weledi wa kutosha hivyo hana shaka kuwa kazi zitaendelea kama kawaida na kuwaomba watumishi kumpa ushirikiano wa kutosha ili aweze kutimiza majukumu yake kikamilifu.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara Prof. Florens Turuka alimkaribisha Dkt. Kihamia na kumuahidi ushirikiano na kwamba wakati wote Bodi itaendelea kutimiza wajibu wake ili Wakala uweze kusonga mbele.


Dkt. Kihamia aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Januari 11,2024 kushika wadhifa wa Mtendaji Mkuu wa DART.