Wafanyabiashara eneo la Simu 2000 watolewa hofu kuhusu ujenzi wa BRT Awamu ya Nne
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Hassan Bomboko amewatoa hofu wafanyabiashara na wadau wa sekta ya usafirishaji wanaohudumu kwenye eneo la Simu 2000 kuwa ujenzi wa Karakana ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Nne kwenye eneo hilo hautoathiri shughuli zao za kila siku.
Bomboko amesema hayo Julai 2,2024 wakati wa kikao kilichoshirikisha Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ubungo, Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Wadau wa sekta ya usafirishaji na Viongozi wa wafanyabiashara wa eneo la Simu 2000 lililoko kwenye Wilaya ya Ubungo.
Awali, akieleza lengo la kikao hicho, Mhe. Bomboko alisema lengo ni kutoa elimu kwa wadau kuhusu ujenzi wa Miundombinu ya Mradi wa DART Awamu ya Nne hususani Karakana ambayo inatarajiwa kujengwa kwenye eneo ambalo kwa sasa linatumiwa na wadau hao.
“Tumekuja kupata ufahamu wa nini kinatarajiwa kufanyika na napenda niwatoe hofu kuwa hakuna mtu yeyote wala kundi lolote ambalo haki yao itavunjwa pale, Serikali yenu ya Wilaya ya Ubungo haiwachukii wafanyabiashara, tuko tayari wakati wote kujadili hoja mbalimbali zinazolenga maslahi yenu na hili linalofanyika ni maelekezo ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu ushirikishwaji wa wananchi kwenye miradi mbalimbali inayowahusu” Amesema Bomboko
Mheshimiwa Bomboko ameongeza kuwa ofisi yake imepokea maelekezo kutoka TAMISEMI kuhusu ujenzi wa Karakana ya Mradi wa DART ambapo imeazimiwa kujengwa kwenye eneo hilo kwa kuwa liko jirani na Miundombinu ya barabara ambapo pia itakuwa rahisi kufikika pindi huduma itakapoanza.
Aidha amewahakikishia wafanyabiashara na wadau hao kuwa ujenzi wa karakana hiyo hautoanza mpaka pale litakapopatikana eneo la muda ambalo watahamishiwa kabla ya kuhamishiwa kwenye eneo la kisasa linalotarajiwa kujengwa mahsusi kwa ajili yao.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa DART, Dkt. Athumani Kihamia amewaondoa hofu wadau hao kuwa wawe na amani kwani ujenzi wa Karakana hiyo hautoleta athari mbaya kwani lengo la Serikali kupitia Mradi wa DART ni kumfikia kila mmoja.
“Hakuna athari yoyote hasi inayoweza kujitokeza, ninyi wenyewe mtajionea”. Amesema Dkt. Kihamia
Dkt. Kihamia pia ameongeza kuwa Wakala wa DART unatarajia kupokea mabasi mapya 177 yatakayosaidia kuondoa kero ya msongamano kwenye Awamu ya Kwanza ya Mradi kutokea Kimara ambapo huduma ya kadi janja pia itaanza kutumika rasmi kwa kuwa zoezi la usimikaji wa mageti limeshakamilika katika awamu hiyo.
Kukamilika kwa Ujenzi wa Karakana ya Mradi wa DART Awamu ya Nne katika eneo hilo kutatoa fursa kwa wafanyabiashara na wadau wengine kwa kuwa eneo tajwa kunatarajiwa kujengwa vyumba vya maduka zaidi ya 150.