Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Wataalamu wa mifumo ya usafirishaji kutoka Hispania watembelea DART
25 Oct, 2023
Wataalamu wa mifumo ya usafirishaji kutoka Hispania watembelea DART

Wataalam kutoka Kampuni ya IDOM ya Nchini Hispania Leo Oktoba 25, 2023 wametembelea Ofisi za Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART).

Lengo la ziara hiyo ni maandalizi ya kujenga na kusimika mfumo nadhifu wa kuongozea magari ‘Intelligence Transportation System (ITS)’ utakaoongeza ufanisi wa huduma ya usafiri kwenye Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka.

Wakiwa katika Ofisi za DART, wataalamu hao wameweza kufahamu mfumo unaotumika hivi sasa katika kuongoza mabasi kwenye Mfumo wa DART, na njia zinazotumika kusimamia na kutatua changamoto za misongamano hususani kwenye makutano. 

Wadau hao pia walipata fursa ya kufahamu mambo mbalimbali yahusuyo Mradi wa DART hususani ujenzi na utekelezaji wa Awamu zote sita za Mradi wa DART.

Katika ziara hiyo Wataalam hao pia walipata fursa ya kufanya kikao na maafisa kutoka Taasisi Wadau wa ITS wakiongozwa DART ambapo wamejadili mambo mbalimbali yatakayosaidia katika utekelezaji wa usanifu na usimikaji wa mfumo huo kwenye miundombinu ya Mradi wa DART.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Meneja wa Uendeshaji wa Miundombinu wa DART, Mhandisi Ahmed Wamala amesema mifumo hiyo ya kuongozea magari inayotaraji kuwekwa ni pamoja na Kamera za usalama (CCTV Cameras), Taa za kuongozea magari ambazo zitafanya kazi kudhibiti na kutoa taarifa zitakazosaidia kufanikisha kazi kwenye Mradi wa DART pamoja na maeneo mengine.

Mhandisi Wamala aliongeza kuwa kupitia ITS, huduma itaboreka  kwani DART itaweza kufahamu mabasi mangapi yanahitajika, maeneo gani yapi yana msongamano pamoja na kutatua kwa haraka changamoto zozote zinazoweza kujitokeza kwenye mfumo wa DART.

Wadau wengine wa Mfumo wa ITS ni Mtoa huduma ya Mabasi (UDART), Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) pamoja na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA).