Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Waziri Kairuki aanza kazi kwa kuitembelea DART
24 Apr, 2023
Waziri Kairuki aanza kazi kwa kuitembelea DART

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Angellah Kairuki, ametembelea Ofisi za Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), ikiwa ni ziara yake ya Kwanza tangu ateuliwe na Mh. Rais Samia Suluhu Hassan kuongoza Wizara hiyo   Oktoba 03, 2022.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Waziri Kairuki alisema ameamua kuanza na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka kwakua ni mradi mkubwa wa kimkakati na wa kipekee ambao sio tu unawahudumia wananchi wengi wa Tanzania bali umekua kivutio kikubwa cha wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani.

“Nimeamua kuanza kazi kwa kutembelea DART kwa kuwa Wakala una umuhimu mkubwa sio tu kwa wana Dar es Salaam lakini hata kwa Kiongozi wetu wa nchi Mh. Rais kwani wananchi wengi na wapiga kura wake na wanategemea huduma ya usafiri kutoka katika mradi huu, hivyo nikaona ni vyema nikaanza majukumu yangu kwa kuja kujifunza na kujionea jinsi DART inavyoendesha shughuli zake,” alisema Waziri Kairuki.

Alisema usafiri wa umma unapokuwa wa uhakika na wa kuaminika shughuli za uchumi wa wananchi zinarahisishwa, na hatimaye wananchi kufurahia matunda ya uwepo wa serikali yao ambayo inawajali.

Katika ziara hiyo, pia Mh. Kairuki alipata fursa ya kutembelea kituo Kikuu cha Mabasi Yaendayo Haraka cha Kimara ambapo alijionea namna wasafiri wanavyotumia huduma ya Mabasi Yaendayo Haraka, huduma za kuhudumia watu wenye makundi maalum, huduma ya Mabasi ya wanafunzi, na pia alitumia fursa hiyo kuzungumza na wananchi na kupata maoni yao juu ya namna bora ya kuboresha huduma zinazotolewa na DART.

Aidha, alitembelea Kituo Kikuu cha Gerezani Kariakoo ambapo alijionea mfumo mpya wa ukusanyaji wa nauli unaojulikana kwa lugha ya Kiingereza Automated Fare Collection System (AFCS) ambao umeongeza makusanyo kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato, sanjari na kupata maelezo ya namna ya kununua tiketi kwa kutumia program tumizi ijulikanayo kwa jina la  Dar City Navigator ambayo inapatikana katika simu janja.

Kwa upande wake, Mtandaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka-DART, Dr. Edwin Mhede alisema anafarijika kuona Waziri ameamua kuanza kazi kwa kuutembelea Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka na kwa kushirikiana na wenzake watahakikisha wanazipatia ufumbuzi wa haraka changamoto zote zinazowakabili wasafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka ikiwemo la kuongeza idadi ya Mabasi.

“Mheshimiwa Waziri nikushukuru sana kwa kuona umuhimu wa kuanza na DART, natambua Tamisemi ni Wizara kubwa ambayo ina majukumu mengi na mazito, kwahiyo umuhimu uliouona kuanza na sisi tmejisikia furaha sana na tunaahidi yale yote utakayoelekeza tutayatekeleza ili kukidhi azma ya Mh.Rais ya kutoa huduma bora ya usafiri wa umma kwa wakazi wa Dar es Salaam,” alisema Dr.Mhede.

Mtendaji Mkuu huyo wa DART alimueleza Waziri Kairuki kuwa, Wakala kwa kushirikiana na Serikali ya Japan kupitia shirika lake la Maendeleo la JICA unatekeleza mpango wa miaka mitatu wa maendelezo yatokanayo na miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka wa Transit Oriented Development (TOD), ambao unalenga kuendeleza maeneo yote ambayo ushoroba wa DART unapita.

Alisema kuwa lengo la mradi huo ni kusaidia wananchi wote ambao miundombinu ya DART inapita karibu nao ili waweze kufaidika kiuchumi na uwepo wa mradi huo, ikiwemo miradi mikubwa ya kibiashara na uwekezaji ambayo itaibuliwa na kufadhiliwa na mradi ili kukuza uchumi wa wananchi katika maeneo hayo.

Akizungumza na vyombo vya habari wakati akihitimisha ziara ya siku mbili katika Kituo cha Gerezani, Waziri Kairuki aliutaka Wakala wa DART kuendelea kuwa wabunifu hasa katika matumizi ya Tehama ili kuendelea kudhibiti mapato ya Serikali pamoja na kuboresha huduma kwa kuongeza idadi ya Mabasi.

Aidha alikemea watu wanaovunja sheria kwa makusudi kwa kuendelea kutumia miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka kinyume na utaratibu, yakiwemo magari ya taasisi mbalimbali na ya watu binafsi kuingilia barabara za Mabasi Yaendayo Haraka, muingiliano wa vyombo vingine vya moto kama pikipiki na bajaji, pamoja na wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga kufanya biashara kwenye miundombinu ya DART.

Ziara ya Mh.Kairuki ilijumuisha pia wakuu wa Wilaya za Ubungo Heri James, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Fatma Almasi, Mkuu wa wilaya ya Ilala Ng’wilabuzu Ludigija pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo.