Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Rais Dkt. Samia Azindua Miundombinu na Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka awamu ya Pili, Awataka wananchi Kulinda Miundombinu.
07 Aug, 2026
Rais Dkt. Samia Azindua Miundombinu na Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka awamu ya Pili, Awataka wananchi Kulinda Miundombinu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt Samia Suluhu Hassan leo Agosti 7, ametembelea na kuzindua miundombinu ya Barabara za mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Pili (BRT II) katika Barabara ya Kilwa, Chang’ombe Sokoine na Kawawa na Kuwataka wananchi kuilinda miundombinu hiyo kwani inajengwa kwa thamani kubwa.

Akizungumza katika viwanja vya ufunguzi eneo la Kwa Azizi Ally Temeke Jijini Dar es Salaam, Mh Rais amesema kila mwananchi ni lazima awe mlinzi namba moja wa mioundombinu ambayo Serikali inaijenga kwa fedha nyingi za Wafadhili na za Walipa kodi ambayo lengo lake ni kuwapunguzia adha ya usafiri wakazi wa Jiji la Dar es Salam na maeneo ya Jirani.

“Mtu yeyote atakayekutwa anahujumu miundombinu hii ni lazima tumchukulie kama mhujumu Uchumi ili miundombinu hii iweze kudumu kwa muda mrefu kwa manufaa ya kizazi hiki na manufaa ya kizazi kijacho” Alisema Mh. Rais.

Aidha Mh.Rais, ameelekeza Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART kuharakisha upatikanaji wa mtoa huduma ya Mabasi katika Awamu ya Tatu ya Mradi unaoelekea Gongo la Mboto kwa kuzingatia mahitaji.

“Niwatake Wasimamizi wa Mradi Huu wenzetu wa DART kuhakikisha wanatafuta kwa haraka mtoa huduma ya Mabasi kule kwenye awamu ya Tatu Gongo la Mboto kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi wa maeneo hayo” Alisema Dkt.Samia.

Mh.Dkt Samia alisema kuanza kwa utekelezai wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Pili sio tu kumewapunguzia adha ya usafiri wakazi wa Mbagala na maeneo ya jirani bali kumeongeza ajira kwa vijana jambo ambalo limeelekezwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

“Nimeona vijana wengi wanafanya kazi za kukatisha tiketi katika Vituo vya Mwendokasi hii ndio tathmini halisi ya maendeleo kwani uwepo wa mradi huu umewawezesha kupata ajira na hatimaye kujipatia kipato” Alisema Dkt.Samia.

Kwa upande wake Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Sid Ould Tah amesema Benki yake itaendelea kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo ambayo inaleta suluhisho la matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi kama ilivyo kwa mradi wa BRT Awamu ya Pili.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Prof Riziki Shemdoe katika salamu zake alimweleza Mh.Rais kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira watahakikisha wanatumia fursa ya matumizi ya Gesi kwenye Mabasi kama chanzo cha mapato.

“Mh.Rais kwa kuwa Mabasi haya yanatumia nishati safi mimi  nitakaa na wenzangu na tutaangalia namna ya kupata fedha kwani tunapunguza sana hewa ya ukaa ambayo ingezalishwa kama Mabasi haya yasingetumia nishati hii ya gesi” Alisema Waziri Shemdoe.

Katika hatua yingine Waziri wa Ujenzi Mh.Abdalah Ulega alimuomba Rais Dkt. Samia barabara zinazoishia Mbagala Rangi Tatu, Gongo la Mboto na Boko kweye awamu za Pili za Tatu na Nne za mradi wa BRT ziongezwe hadi kufikia maeneo ya Vikindu,Kisarawe,Bagamoyo na Kibaha ili miundombinu hiyo iweze kuunganisha Mkoa wa Dar es Salaaam na Pwani jambo ambalo Mh Rais alilikubali.